Tafuta katika Blogu Hii

Jumapili, 7 Desemba 2014

UFAHAMU UGONJWA WA ZINAA WA CHLAMIDIA,DALILI ZAKE ,MADHARA,TIBA NA KINGA


Chlamidia ni aina ya ugonjwa ulio katika kundi la magonjwa ya zinaa(STD) unaosababishwa na bacteria aina ya CHLAMIDIA TRACHOMATIS,ambao wanaweza kuathiri viungo vya uzazi na pia kusababisha ugonjwa wa homa ya mapafu unaojulikana kama TYPICAL PNEUMONIA.Kati ya magonjwa ya zinaa yanayosababishwa na bakteria,chlamidia ndio ugonjwa unaoongoza kwa maambukizi duniani ambapo nchini Marekani pekee inakisiwa watu milioni 4 huambukizwa ugonjwa huu kila mwaka.
  Inawezekana jina la ugonjwa huo halijazoeleka katika masikio ya wengi na hii huenda ni kutokana na kutokuwepo kwa takwimu za kutosha kuhusiana na suala hilo katika nchi nyingi barani Afrika na hasa katika nchi zetu za Afrika Mashariki,hivyo ni vigumu kujua idadi kamili ya maambukizi.Lakini bila shaka chlamidia ndio ugonjwa wa zinaa unaotokana na bakteria unaoongoza kwa maambukizi mengi zaidi duniani ukifuatiwa na ugonjwa wa gono.Gonjwa hili ambalo huwaathiri wanawake na wanaume pia linaweza kuleta madhara makubwa ikiwa ni pamoja na kuharibu mfumo wa uzazi wa mwanamke.
  Nchini Marekani pekee mwaka 2011 kesi milioni 1 na nusu ziliripotiwa katika hospitali katika majimbo 50 ya nchi hiyo,katika hali ambayo kesi nyingi hazikuripotiwa kwa kuwa watu wengi wenye kuambukiza ugonjwa huo huwa hawaonyeshi dalili na hivyo hawakwenda hospitali.Kama yalivyo magonjwa mengi ya zinaa,chlamidia pia huwapata zaidi vijana na takwimu zinaonyesha kuwa kati ya wasichana walio na umri wa miaka 14-15 wenye kufanya ngono zembe mara kwa mara,mmoja wao huambukizwa chlamidia.
   Ugonjwa wa chlamidia huweza kuambukizwa kupitia njia za kujamiiana .Mtu yoyote mwenye kufanya ngono zembe na mtu aliye na ugonjwa huo anaweza kuambukizwa.Pia mama mjamzito huweza kuambukiza mtoto wake wakati wa ujauzito.Vilevile ugonjwa huo wa zinaa unaweza kuambukizwa kupitia mbwa,vinyesi vya wanyama kama vile ndege walioambukizwa aina ya chlamidia inayopatikana kwa wanyama kwa mfano kuku,bata,kasuku na kadhalika na kusababisha aina ya homa ya mapafu inayojulikana kama PSITTACOSIS ambayo huambatana na homa kali yenye nyuzi joto kati ya celsius 39.4 hadi 41.1.Chlamidia huathiri sehemu tofauti za mwili wa binadamu kama macho,mfumo mzima wa kupumua,sehemu za siri,viungo vya uzazi na tezi(lymph nodes)

     DALILI NA VIASHIRIA VYA UGONJWA WA CHLAMIDIA
 -Asilimia 75 ya wanawake na asilimia 50 ya wanaume wanaopata maambukizi ya ugonjwa huu huwa hawaonywshi dalili zozote za ugonjwa huo ila dalili hutokea baada ya wiki 1-3 baada ya mtu kupata maambukizi.

   DALILI KWA WANAWAKE;
1)Kutokwa na majimaji ya rangi ya njano yanayotoka kwenye utupu,ambayo huwa na harufu kali
2)Kuhisi maumivu wakati wa haja ndogo
3)Kuhisi kama kuwaka moto wakati wa kukojoa
4)Kutokwa na damu katikati ya kipindi cha hedhi yaani baada ya kumaliza mzunguko wa hedhi na kabla ya kuanza mzunguko mwengine
5)Kuhisi maumivu sehemu ya chini ya tumbo
6)Kuhisi maumivu wakati wa kujamiiana
7)Kutokwa na damu wakati wa kujamiiana na pia kuvimba na kuhisi maumivu kwenye tezi zilizopo sehemu za siri

   DALILI KWA WANAUME;
1.Kuhisi maumivu wakati wa kukojoa
2.Kuhisi kama kuwaka moto wakati wa kukojoa,
3.Kutokwa na njimajikwenye uume ambayo yanaweza kuwa ya ragi nyeupe kama maziwa,kijivu au rangi ya njano.
4.Sehemu ya tundu kwenye uume kuwa nyekundu,kuvimba na kuwasha.
5.Kuhisi maumivu kwenye korodan na tezi zilizopo sehemu za siri ambazo huvimba na huambatana na maumivu.Mara nyingi dalili hizi kwa wanaume huja na kupotea au zinaweza kuonekana tu wakati anapoenda kukojoa asubuhi baada ya kuamka kutoka usingizini.
-Dalili za ugonjwa huu kama umeathiri puru(rectum) kwa wanawake na wanaume ni kama ifuatavyo;
     a)Kuwashwa na kutokwa na damu kwenye puru
     b)Maumivu wakati wa kujisaidia haja kubwa
     c)Kutokwa na uchafu kama kamasi kwenye puru(rectum)
Iwapo vimelea vya chlamidia vitaathiri macho,wanawake na wanaume huwa na dalili zifuatazo;
 -Uvimbe kwenye macho
 -Macho kuwa mekundu
 -macho kuwasha na hata kutokwa na majimaji machoni.
Baada ya mtu kuhisi dalili hizo tulizozitaja ,hupaswa kwenda hospitalini au katika kituo cha afya ili kupimwa na kuthibitishwa kwamba ana ugonjwa huo ili apatiwe matibabu.
  Vipimo vya uchunguzi vya ugonjwa wa chlamidia ni Urethral swab for culture.Katika kipimo hiki majimaji kutoka kwenye uume au uke huchukuliwa kwa kutumia kijiti chenye pamba au swab maalum ambayo hupelekwa maabara ili kuoteshwa na kuangalia aina ya uoto wa bakteria.Pia huchukuliwa vipimo vya mkojo na pia kipimo cha PCR au Polymerase Chain Reaction,ambacho ni cha kuangalia vinasaba vya bakteria au DNA na hufanywa katika maabara.Baada ya majibu kuonyesha kuwa mgonjwa ameambukizwa vimelea vya ugonjwa huo matibabu hufuata.Chlamidia ni kati ya magonjwa ya zinaa yanayotibika na ugonjwa huu hutibiwa kwa dawa aina ya antibiotiki zilizopo kwenye makundi ya macrolides,Quinolones na Polyketides ambazo hutolewa chini ya maelekezo ya daktari.

 MADHARA YA UGONJWA WA CHLAMIDIA;
  Kwa wanaume;
-Huathiri korodani na kusababisha mwanaume kukosa uwezo wa kuwa na watoto au kuwa tasa na pia husababisha maambukizi kwenye tezi dume(prostates).
Kwa wanawake;
-Husababisha maambukizi kwenye mirija ya uzazi,mfuko wa uzazi na mayai ya uzazi,kwahivyo kusababisha ugonjwa wa uvimbe katika fupanyonga au Pelvic inflammatory disease(PID).Pia huongeza uwezekano wa wanawake kupata mimba zilizotunga nje ya mfuko wa uzazi ambazo kitaalam huitwa Ectopic pregnancy.Mbali na hilo,mwanamke hupata maumivu sugu kwenye nyonga na ugonjwa wa mifupa arthritis aina ya Reiters syndrome.
-Vilevile chlamidia huweza kusababisha ugumba kwa mwanamke kama hatapata tiba.Si hayo tu,kwa wanawake wajawazito chlamidia husababisha wajifungue kabla ya wakati wake.Pia mtoto anaweza kuzaliwa na maambukizi kwenye masikio,sehemu za siri,macho,mapafu (homa ya mapafu),na kama mtoto hatopatiwa tiba ya haraka ya macho baada ya kuzaliwa basi anaweza kuwa kipofu.
-Dalili za chlamidia kwa watoto wachanga hutokea katika kipindi cha wiki 2 kwenye macho,na iwapo ni homa ya mapafu dalili zake hujitokeza katika kipindi cha wiki 2-miezi 3 baada ya kuzaliwa.

  NJIA ZA KUJIKINGA NA UGONJWA WA CHLAMIDIA;
-Kwa wanawake wajawazito,ni vizuri kuhudhuria klinik mapema wakati wa ujauzito na kupima vipimo mbalimbali ambapo kimojawapo ni cha kuangalia iwapo mama mjamzito ameathirika na ugonjwa huu ili aweze kupatiwa matibabu mapema
-Kwa wenye maambukizi wanashauriwa kuchukua tahadhari ya kutowaambukiza wapenzi wao kwa kufanya ngono salama,pia kuepuka kushika macho kwa kutumia mikono na hata ikiwezekana kuwaepuka wapenzi wao ili kuwalinda na maambukizi.
-kwa  wale ambao wapenzi wao wameambukizwa au wameonyesha dalili za ugonjwa huu,wanashauriwa na wao pia kupata tiba hata kama hawana dalili zozote pia kondom zihusike kwa kila tendo la ndoa.

NB;Njia kuu na sahihi ya kujikinga na magonjwa ya zinaa ni kuacha au kuepuka kujamiiana au kufanya ngono zembe na zisizo salama.

MOBL;+255776 217 417
fax2email+255 736 601119
email;lmtmherbal@rocketmail.com